ASASI ZAIPONGEZA SERIKALI UTEKELEZAJI WA HAKI ZA BINADAMU NCHINI.
Asasi za Kiraia na Haki za
Binadamu zimeeleza kuridhishwa na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika
kutekeleza Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu pamoja na Itifaki ya
Maputo.
Pongezi hizo zimetolewa wakati
wa kikao kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Machi 19 hadi 21,
2025, ambapo wadau wamekutana na kujadili maendeleo ya utekelezaji wa mkataba
huo.
Akizungumza katika kikao hicho
Wakili Laetitia Ntagazwa, Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS), amesema kuwa miongoni mwa mambo yanayosaidia katika kuimarisha Utawala
wa Haki nchini ni pamoja na amani iliyopo jambo ambalo kila Mtanzania anapaswa
kujivunia.
Wakili Laetitia aliongezea
kuwa licha ya Tanzania kumpoteza Kiongozi wa Nchi aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano
Hayati John Pombe Magufuli, bado nchi ya Tanzania ilifanikiwa kufanya
mabadiliko ya Uongozi kwa amani na utulivu jambo ambalo linaonesha taswira
nzuri kwa nchi katika kusimamia na kudumisha amani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Msaidizi wa Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Beatrice
Mpembo, aliongeza kuwa kikao kazi hicho kitasaidia kuboresha rasimu ya mkataba
huo na pia kutoa nafasi ya kujitathmini kama Taifa kuhusu hali ya utekelezaji
wa Haki za Binadamu Nchini.
Comments
Post a Comment