Thursday, September 24, 2020

MAZUNGUMZO YA AMANI YATAJWA KUWA NJIA BORA NA SALAMA YA UTATUZI WA MIGOGORO NCHINI.
 
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Mazungumzo ya amani ni muarobaini uliothibitika kutumika kama tiba ya migogoro ya ardhi Mvomero Mkoani Morogoro.

 

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Albinus Mgonya wakati akitoa taarifa ya hali ya amani wilayani humo kwa Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliyofika walayani kwake hivi karibuni.

 

Wakulima na wafugaji ni watanzania wanaoishi pamoja na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi katika maeneo wanaoishi na zaidi, wengi wao ni wakulima na ni wafugaji kwa wakati mmoja hivyo njia ya mazungumzo ya amani imejipambanua kuwa tiba ya utatuzi wa migogoro inayowakabili.

 

"Unajua, hawa wakulima na wafugaji wanafahamiana kwasababu wanaishi pamoja, matumizi ya nguvu hususani vyombo vya ulinzi na usalama isingekuwa muarobaini, badala yake kwa kuwakutanisha na kuzungumza nao kumeonesha kuwa ni suluhisho la migogoro na ujenzi wa amani na utulivu baina yao."

 

Kwa niaba ya wakulima na wafugaji ndugu Moringe Kwinasei ameungana na Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuthibitisha hali ya uwepo wa utulivu na amani uliotokana na utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo ya amani na kuwataka wakulima na wafugaji kuacha tabia ya uchochezi kwa kisingizio cha migogoro baina yao.

 

"Unajua sisi ni ndugu na wote tunahitajiana katika mambo mengi ikiwemo mazao ya mifugo na mimea ambayo ndiyo yanatugombanisha, tunagombana shambani baadae tunakaa hotelini tunakula wali-nyama! sasa kwanini tuendelee kugombania mambo ambayo ni sehemu ya mahitaji yetu muhimu? Ameongeza kwa kuuliza Martine Matingise.

 

Aidha, Mhe. Mgonya amesema Wilaya yake imeanzisha programu ya michezo mbalimbali hasa mashindano ya mipira wa Miguu kati ya Wakulima na wafugaji,  mbinu hii imeonesha kuwa na tija katika ujenzi wa amani katika Wilaya hiyo kwasababu michezo imewaleta wakulima na wafugaji pamoja na kuishi kwa upendo.

 

"Nimeanzisha na kuhamisisha michezo mbalimbali hasa mpira wa Miguu kati ya wakulima na wafugaji, na nimekuwa nikishiriki nao katika michezo husika. Kwakweli njia hii pia imeonesha mafanikio makubwa katika jitihada za Serikali katika ujenzi wa amani na kuzuia migogoro katika jamii." Amemaliza Mhe. Mgonya.

 

Kamati hii imehitimisha ziara yake ya utekelezaji wa majukumu muhimu ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari katika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro baada ya kufanya kazi kama hiyo katika Mikoa ya Arusha, Manyara na Rukwa.

 


Monday, September 21, 2020

PROF. MCHOME ATAKA WATANZANIA KUTUMIA VIZURI RASILIMALI ZILIZOPO NCHINI ILI KUJILETEA MAENDELEO


Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome akifungua kikao cha Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi cha kujadili Mfumo Jumuishi wa Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Rasilimali za Nchi kilichofanyika jijini Arusha.

Washiriki wakichangia mada katika kikao cha Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi cha kujadili Mfumo Jumuishi wa Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Rasilimali za Nchi. 
Washiriki wakiendelea na kikao.


Washiriki wa kikao wakiwa katika picha ya pamoja.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX


Nchi ya Tanzania imebarikiwa utajiri wa asili na rasilimali asilia ambazo zikitumika ipasavyo nchi na wananchi wake watakuwa na maendeleo ya kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome wakati wa kikao cha Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi za Serikali waliokutana jijini Arusha kujadili Mfumo Jumuishi wa Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Rasilimali za nchi.

Profesa Mchome alisema Sheria ya Usimamizi wa Utajiri wa Asili na Maliasilia ilitungwa ili kuweza kusaidia kulinda rasilimali zilizopo nchini ili ziweze kuwanufaisha wananchi wake.

Alisema “Utajiri wa Asili na Maliasilia zinatakiwa zitumike kwa manufaa ya nchi na watu wake na sio kwa manufaa ya nchi za nje, mwaka 2017 tulitunga sheria ambayo ilisaidia kuweka miongozo jinsi gani tuenende katika eneo hilo na jinsi gani watu watafaidi  kutokana na maliasilia zao  na utajiri ambao upo katika nchi yao”.

Alisema, Wawekezaji wadogo wameanza kuongezeka na kufanya shughuli za uzalishaji kwa vibali halali na kwa uhuru bila kukimbizwakimbizwa na hivyo kuongeza pato la nchi.

Profesa Mchome alisisitiza, kwa sasa ardhi inatumika vizuri haitumiki kwa mtu mmoja kushika eneo kubwa bila manufaa yoyote kwa wananchi sasa ardhi inatumika na kuwapatia wananchi manufaa ambayo wanahitaji katika makazi, kilimo na maeneo mengine kwa hiyo malalamiko yameanza kupungua na wananchi wameanza kuwa wamiliki wa ardhi ambao ni utajiri wa asili na mali asilia unaozungumziwa.

Katibu Mkuu wizara ya katiba na sheria ,Profesa Sifuni Mchome amesema kuwa,endapo nchi yetu itazitumia rasilimali tulizonazo itasaidia sana kuharakisha shughuli za maendeleo Kama zilivyo kwa nchi zingine ambazo uchumi wao umeweza kukua kutokana na matumizi mazuri ya rasilimali hizo.

Aidha, Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Saalam (UDSM),Dokta Abel Kinyondo alisema kuwa,Kuna njia mbili za kuhakikisha wananchi wananufaika na Kodi na tozo mbalimbali zinazotokana na maliasili zetu  serikali inazitumia kwa namna ya kimkakati kuwarudishia wale walioko chini kabisa waweze kunufaika nazo.

Dokta Kinyondo alisema kuwa ,lazima tujue kuwa kwenye kufaidika zaidi na kwenye hela zaidi sio kwenye tozo na Kodi bali wananchi waunganishwe moja kwa moja katika mnyororo wa thamani katika maliasili kwani sehemu kubwa ya mapato inatokana na rasilimali.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkaazi wa UNDP, Bi Christine Musisi ambao ndio wafadhili wa kikao hicho, alisema wapo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa na kunufaisha wananchi wake.

 


Monday, September 14, 2020

MAADILI KWA WATUMISHI WA UMMA NI TIBA YA AMANI NCHINI

 XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Usimamizi thabiti wa maadili kwa watumishi wa umma katika kata na vijiji mkoani Morogoro umetajwa kuwa sababu ya kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

 

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Eng. Emmanuel N.M. Kalobelo alipotembelewa ofini kwake leo na Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari.

 

Eng. Kalobelo amesema ukosefu wa maadili kwa watendaji wa kata na vijiji umeonekana kuwa kichocheo cha migogoro na uvunjifu wa amani katika maeneo mengi nchini lakini Serikali chini ya Mhe. Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli imefanya kazi kubwa ya kulikomesha tatizo hilo mkoani Morogoro.

 

"Siku za nyuma Mkoa wa Morogoro ulikuwa kati ya mikoa yenye migogoro mingi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji lakini baada ya kufanya utafiti wa kina tukagundua watendaji na viongozi wa kata na vijiji walikuwa ndiyo chanzo kwani waliidhinisha uuzaji wa maeneo yasiyopimwa bila kufuata taratibu sahihi." Amesema Eng. Kalobelo.

 

Baada ya kubaini kinachofanyika na watendaji hao, Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo husika tumesimamia kwa nguvu maadili kwa kutumia mbinu mbalimbali kwa mafanikio na sasa wanafanya kazi zao kiweledi jambo lililopunguza tatizo kwa kiasi kikubwa.

 

Aidha Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Morogoro amesema wameendelea kushughulikia na kusimamia upimaji wa ardhi pamoja na ugawaji wa maeneo husika ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji kupunguza migogoro ya ardhi katika mkoa huo na Wilaya zake.

 

"Kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tumeanzisha Ofisi ya kusimamia Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ulisaidia kupima maeneo na kusimamia ugawaji wake kwa kuyatenganisha ili wakulima wawe na maeneo yao na wafugaji pia wawe na maeneo yao, mpango huu umesaidia kuzuia muingiliano wa shughuli za kilimo na  ufugaji." Ameongeza Eng. Kalobelo.

 

Kamati hii ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliundwa mwezi  Februari, 2012 chini ya Itifaki ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari  iliyoridhiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mkataba wa nchi za Maziwa Makuu wa Usalama, Utulivu na Maendeleo (The Pact on Security, Stability and Development in the Great Lakes Region).

 

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Felistas Mushi wa Wizara ya Katiba na Sheria inaundwa na Wataalamu wanne ambao ni Miraji Magai Maira wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere ambaye pia ni Katibu wa Kamati, Saleh Ambika wa Wizara ya Mambo ya Ndani (Jeshi la Polisi), Lina Kitosi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Pius Katani kutoka Ofisi ya Rais Ikulu.

 

Kamati hiyo  ya watalaamu watano imefika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kuonana na Katibu Tawala Eng. Emmanuel Kolobelo kabla ya kuelekea Mvomero kukagua utekelezaji wa masuala ya Ujenzi wa Amani inayohusisha rasilimali na hatimaye kusababisha mapigano na hata mauaji kati ya wakulima na wafugaji, wawekezaji na wananchi na wakati mwingine wananchi wenyewe kwa wenyewe.

 

 


WATUMISHI WIZARA YA KATIBA NA SHERIA WASISITIZWA KULINDA MALI ZA UMMA


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome ambaye ni mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi la wizara hiyo akiongoza mkutano huo katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.


Wajumbe wa baraza la wafanyakazi la Wizara ya Katiba na Sheria wakiendelea na mkutano huo.


Zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa Katibu wa baraza likiendelea.


Katibu wa Baraza la wafanyakazi Wizara ya Katiba na Sheria Bi Basuta Milanzi (kushoto) akiwa na Katibu Msaidizi wa Baraza hilo Bw. Felix Chakila baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hizo.


Naibu Katibu Mkuu Ndg. Amon Mpanju akiwa amegusa kwa fimbo mchanga unaohama.


Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakiwa mbele ya mchanga unaohama.

Nyumbu ni moja ya wanyama ambao ni vivutio vilivyopo katika bonde la Ngorongoro.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX


Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wametakiwa kulinda mali za umma kama za kwao binafsi ili ziweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.

Maelekezo hayo yametolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome ambaye pia ni Mwenyekiti wa  Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo wakati akifungua mkutano wa Baraza hilo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro jijini Arusha.

“Watumishi wote tunatakiwa kulinda mali za umma kama za kwetu binafsi na kuzitumia kwa uangalifu mkubwa ili ziweze kudumu kwa muda mrefu”Alisema Prof. Mchome

Aidha, Prof. Mchome aliwaasa watumishi hao kuwa waadilifu kwa kutokunywa pombe wakiwa kazini, madereva wasibebe abiria njiani wanapokuwa safarini, pia watumishi wasiondoke na vifaa vya ofisi kwenda navyo nyumbani.

Mbali na hayo, Prof. Mchome alizitaka Idara na Vitengo katika Wizara hiyo kuwa na utaratibu endelevu wa kufanya vikao vya ndani mara kwa mara ili kubaini na kutatua changamoto zilizopo ndani ya Idara na Vitengo na kuepuka malalamiko kutoka kwa watumishi wa chini.

Alisema ,“Idara na Vitengo viwe na utaratibu endelevu wa kukaa vikao vya ndani ili kujua na kutatua changamoto mbalimbali zilizopo ndani ya Idara na Vitengo vyenu”.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ndg. Amon Mpanju aliwaeleza watumishi ambao ni wajumbe wa baraza hilo kurudi kwenye misingi ya utumishi wa umma na kuvaa ipasavyo kwa kuzingatia waraka wa mavazi uliotolewa na Manejimenti ya Utumishi wa Umma.

“Watumishi mnatakiwa mrudi kwenye misingi ya utumishi wa umma kwa kuzingatia waraka wa mavazi uliotolewa na menejimenti ya utumishi wa umma na sio mtumishi kuvaa mavazi yasiyostahili kwenye utumishi wa umma”, alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Katika mkutano huo wajumbe walipata nafasi ya kusikiliza mada mbili ambazo ni haki na wajibu wa mjumbe wa baraza la wafanyakazi pamoja na wajibu wa chama cha wafanyakazi katika baraza la wafanyakazi na mahala pa kazi iliyotolewa na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Manyara Bw. Samwel Said na mada ya pili  ilikuwa ushirikishwaji wa wafanyakazi iliyotolewa na Afisa kazi Mkuu Mfawidhi Mkoa wa Manyara Bw. Perfectos Kimaty.

Awali kabla ya kuanza kwa mkutano huo wajumbe walipata nafasi ya kuchagua Katibu wa Baraza na Katibu Msaidizi kwani waliokuwepo wamemaliza muda wao. Katika uchaguzi huo Bi Basuta Milanzi alichaguliwa kuwa Katibu wa Baraza hilo baada ya kumzidi mshindani wake Bw. Felix Chakila ambaye alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi.

Mbali na kikao hicho, wajumbe walipata nafasi ya kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea hifadhi ya Ngorongoro na kujionea vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo ikiwemo wanyama kama vile Nyumbu, Pundamilia, Faru na pia kuona mchanga unaohama.

 Tuesday, September 8, 2020

KASI YA MAENDELEO YATAJWA KUWA KICHOCHEO CHA AMANI NCHINI
 


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Kasi ya maendeleo yatajwa kuwa kichocheo cha amani nchini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule alipotembelewa na Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari ofisini kwake leo.

 

Dkt. Haule ametaja mafanikio yaliyofanywa na Rais wa Awamu ya Tano Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli katika Sekta za Afya, Elimu, Barabara, Umeme, Maji na upatikanaji haki kwa wakati kuwa ni kichocheo cha ujenzi wa amani na utulivu hapa nchini.

 

"Huduma za jamii kama maji, elimu, umeme, afya, usafiri na usafirishaji ni haki ya msingi ya kila mwananchi. Naipongeza Serikali yangu chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuyapa kipaumbele masuala haya muhimu katika ujenzi wa amani na uchumi wa Taifa kwa kwa ujumla" amesema Dkt Haule.

 

Mwananchi akipata haki ya maendeleo kwa kuboreshewa na kusogezewa karibu huduma za jamii na nyingine hawezi kujihusisha na migogoro yoyote katika jamii kwani akili yake inakuwa imetulia, hivyo kujielekeza katika kufanya shughuli za maendeleo na kujipatia kipato, ameongeza Dkt. Haule.

 

Hata hivyo, Dkt. Haule ameiomba Serikali kuendelea kuweka mkazo na juhudi katika kuhakikisha huduma za jamii zinawafikia wananchi wote katika maeneo yao kama inavyojieleza katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025.

 

Kwa upende wake Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari Bwn. Miraji Magai Maira wakati akimshukuru Mkuu huyo wa Wilaya ya Sumbawanga amesema wanalazimika kufika kwa wananchi na kukutana na makundi mbalimbali ya vinaja, wafugaji, wakulima, Walemavu, viongozi wa Mira na viongozi wa dini kwasababu huko ndiko migogoro inakoanzia na isiposhughulikiwa kwa wakati huhatarisha amani ya nchi.

 

Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliyoanzishwa Februari, 2012 chini ya itifaki ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari na kuridhiwa na serikali ya Tanzania kupitia Mkataba wa nchi za Maziwa Makuu wa Usalama, Utulivu na Maendeleo itaendelea na mkakati wa utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya kujenga na kudumisha amani na utengamano kwa kufanya vikao vya ujenzi wa amani kwa siku mbili katika mkoa wa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga na baadae kumalizia vikao hivyo mkoani Morogoro.